Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewatoa hofu Watanzania kwa kusema kuwa tishio la virusi vya ugonjwa wa corona halijaathiri upatikanaji wa mafuta (petroli, dizeli, mafuta ya taa) nchini.
Dkt. Kalemani amesema hayo jijini Dar es Salaam alipotembelea bandari ili kujiridhirisha kama kuna mafuta ya kutosha kukidhi mahitaji yanayohitajika nchini, na kusema kuwa kuna ziada ya mafuta itakayotumika zaidi ya siku 30 na bado meli zinaendelea kupakuwa mafuta bandarini.
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuna mafuta ya kutosha siku zote ili miradi mikubwa ya kitaifa inayoendelea kutekelezwa kama vile ya SGR, Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere, miundombinu ya barabara, maji na mingine mingi isikwame kwa kukosa mafuta kutokana na ugonjwa huo.
“Ninawahakikishia Watanzania kwa niaba ya serikali kuwa mafuta yapo na yataendelea kuwepo, tumshukuru Rais wetu, Dkt. John Magufuli kwa msimamo wake thabiti kwani anatuwezesha kufanya kazi usiku na mchana, hivyo hatutaweza kuathirika kwa yanayosemwa, tumekaa na wadau pamoja na wataalamu wetu tumeweka mpango na mikakati ya kuhakikisha mafuta yanapatikana muda wote,” amesisitiza Dkt. Kalemani.
Katika hatua nyingine, amewasihi wawekezaji kuja kufanya tafiti na kuwekeza katika sekta ya mafuta, kwa kuwa bei ya mafuta katika soko la dunia inaendelea kuongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma, na kueleza kuwa mwaka jana pipa la mafuta ghafi lilikuwa dola 50, ambapo kwa sasa ni dola 57, mafuta safi ilikuwa dola 278, na sasa ni wastani wa dola 446.
Katika ziara hiyo ametoa onyo kwa baadhi ya wananchi kuacha tabia ya kuhujumu miundombinu ya mafuta, na kueleza kuwa ikitokea mtu amekamatwa kwa kosa hilo ahukumiwe kama wahujumu uchumi wengine kulingana na sheria za nchi.