Watoa Huduma Ndogo ya Fedha watakiwa kujisajili na kukata leseni

0
394

Serikali imewataka watoa huduma ndogo za fedha kujisajili na kukata leseni kabla ya tarehe 31 Oktoba, 2020, kipindi ambacho ni cha mpito kilichowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2019 kabla ya Sheria hiyo kuanza kutumika rasmi kuanzia tarehe 1 Novemba, 2020.

Rai hiyo imetolewa Mjini Morogoro na Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja, kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bw. Adolf Ndunguru wakati akifungua mpango wa utoaji elimu kwa umma kuhusu Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha kwa wadau wa Sekta hiyo kutoka Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa.

Dkt. Mwamwaja alisema lengo la kusajili na kutoa leseni kwa watoa huduma hao ni kuiwezesha Serikali kuwatambua watoa huduma hao ili kuboresha usimamizi na udhibiti wa Sekta Ndogo ya Fedha nchini na kuwa na Sekta ya Fedha iliyo endelevu na yenye kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini kwa kuwa sekta hiyo ni muhimu katika uchumi wa nchi.

“Sekta hii inatoa huduma za fedha kwa wananchi wa kipato cha chini ambazo zinachangia kuinua uchumi na kuongeza kipato, kwa mujibu wa utafiti wa Finscope wa mwaka 2017, asilimia 55.3 ya nguvukazi ya Taifa wanapata huduma za fedha kutoka Taasisi za Huduma Ndogo za Fedha”, alisisitiza.

Alisema kutokana na umuhimu huo Serikali imekuwa ikitoa elimu ya kuwawezesha wananchi kutekeleza Sheria hiyo na mpango wa utoaji elimu hiyo kuzinduliwa rasmi Desemba, 2019 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ambapo sasa elimu hiyo inaendelea kutolewa kwa wadau wa Kanda ya Kati.

“Serikali itahakikisha elimu hii inaendelea kutolewa nchi nzima ili kuhakikisha wadau wote muhimu wanafikiwa na elimu hii na kuwawezesha kufuata matakwa yote ya Sheria kwa maendeleo ya uchumi wa nchi”, alisema.

Dkt. Mwamwaja aliwataka wadau hao kuwa mabalozi wazuri wa kuwafundisha wadau wengine elimu hiyo kwa ufasaha huku akiwatahadharisha kuepuka upotoshaji ili kufanikisha utekelezaji wa Sheria hiyo.

Naye Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Dionisia Mjema alisema Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kisera na kisheria ili kuweka mazingira wezeshi ya uendelezaji na ukuaji wa sekta ya fedha ikiwemo Sekta Ndogo ya Fedha.

Alisema kutungwa kwa Sheria hiyo ni miongoni wa jitihada zinazochukuliwa na Serikali kwa ajili ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizokuwa zinaikabili Sekta ya Fedha ikiwemo utoaji wa mikopo kwa masharti magumu pamoja na kutoza riba kubwa.

Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha inazitambua taasisi za huduma ndogo za fedha katika maDaraja manne ambayo ni Daraja la kwanza linalohusisha taasisi za huduma ndogo za fedha zinazopokea amana, Daraja la Pili linahusisha taasisi za huduma ndogo za fedha zisizopokea amana ikiwemo wakopeshaji binafsi, watoa huduma kwa njia kielekroniki na kampuni za mikopo, Daraja la Tatu ni Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) na Daraja la Nne ambalo ni vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha kama vile VICOBA, VSLA.

Alisema kuwa Sheria hiyo inasimamia Daraja la pili, la tatu na la nne ambapo watoa huduma katika Daraja la pili watatakiwa kukata leseni ya kufanya biashara ya huduma ndogo za fedha Benki Kuu ya Tanzania. Aidha, watoa huduma wa Daraja la tatu watakata leseni za kufanyabiashara katika Tume ya Maendeleo ya Ushrika Tanzania na wale wa Daraja la nne watajisajili katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo waliishukuru Serikali kwa kutoa mafunzo hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yatasaidia kuondoa hofu iliyokuwepo miongoni mwa wananchi hususani watoa huduma katika Daraja la nne kutokana na taarifa mbalimbali za upotoshaji zilizokuwa zikiendelea katika mitandao ya kijamii kuhusu uwepo wa Sheria hiyo.

Mkurugenzi wa Taasisi ya TIMAP, Bw. Abubakar Othamn ni miongoni mwa washiriki hao alisema elimu hii imeanza kutolewa wakati muafa na kuiomba Serikali kuongeza nguvu zaidi katika utoaji wa elimu hiyo ili wananchi wote waweze kutekeleza matakwa ya Sheria.