Wasafiri kutoka nchi zilizoathirika na corona kujitenga kwa siku 14

0
386

Rais John Magufuli ametangaza kuanzia kesho Machi 23, wasafiri wote watakaongia nchini kutoka kwenye mataifa yaliyoathirika zaidi na virusi vya corona , watalazimika kufikia sehemu za kujitenga na kukaa huko kwa muda wa siku 14 kwa gharama zao.

Amesema tangazo hilo linawahusu pia Watanzania wanaotoka kwenye nchi hizo ambao walikwenda kwa shughuli mbalimbali.

Rais Magufuli ametoa tangazo hilo wakati akihutubia Taifa kuhusu virusi hivyo vya corona.

Kwa upande wa serikali, Rais Magufuli amesema kuwa kuanzia sasa imesitisha kutoa vibali vya kusafiri kwa watumishi kwenda kwenye nchi hizo zilizoathirika na virusi vya corona.

Amewasihi Watanzania ambao hawana shughuli za lazima sana za kutembelea nchi hizo, pamoja na maeneo mengine, yakiwemo ya ndani ya nchi, kuahirisha safari zao kwa sasa.

Halkadhalika ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na mamlaka nyingine husika, kuhakikisha maabara ya Taifa inaimarishwa kwa kupatiwa vifaa vya kisasa vya uchunguzi ili kuweza kuwabaini kwa haraka watu walioambukizwa virusi vya corona

Aidha, ameagiza maeneo yote ya vituo vinavyotumiwa na watu kuingia nchini, yapelekewe vifaa vya ukaguzi na vile vya kuwakinga watumishi wa vituo hivyo dhidi ya virusi vya corona.