Serikali imetambua rasmi kundi la wamachinga kama kundi maalum na kuwekwa chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Akizungumza na viongozi wa wamachinga Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan, amesema imefika wakati kundi hilo kutambulika rasmi kutokana na utendaji kazi wanaoufanya pamoja na kuajiri vijana wengi nchini.
“mwanzoni nilikuwa nasita kidogo kutumia jina hili, labda niliona jina linalofaa ni wafanyabiashara ndogondogo, lakini kumbe hili jina la wamachinga mnalipenda na linafaa kutumika”,- amesema Rais Samia Suluhu Hassan.
Pia Rais Samia amesema amemwamuru mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla, kuwarudisha katika soko la Karume wamachinga hao huku serikali ikiendelea kujenga masoko yenye hadhi kote nchini.
“Juzi nilipokutana na mkuu wa mkoa nikamwambia nendeni wekeni mpango mzuri, lakini acha wamachinga warudi Karume, niliamua hivyo nikijua kwamba kukaa kwenu nje kuna changamoto nyingi biashara haifanyiki, familia zinasubiri, nikasema pamoja na kwamba tuna lengo la kujenga masoko mazuri lakini acha kwa sasa wajijengee warudi”,-amesema Rais
Kwa upande wake mwakilishi wa wamachinga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Wamachinga Taifa, Steven Lusinde amemuomba Rais Samia kuendelea kuboresha miundombinu ya masoko ili waweze kufanya kazi vizuri.
“Masoko mengi hayana miundombinu, kwa hiyo tukuombe mheshimiwa Rais msaidie [msupport] kuhakikisha kwenye maeneo ambayo tumekwenda tunapata maji, barabara, vyoo, n.k,”-amesema Lusinde.