Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema ujenzi wa majengo mapya katika chuo cha ualimu Kabanga kilichopo mkoani Kigoma, ni moja ya mikakati ya Serikali yenye lengo la kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu nchini.
Akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa majengo hayo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma, DKt Mpango amesema lengo la Serikali kujenga majengo hayo ni kukiwezesha chuo hicho cha ualimu cha Kabanga kudahili Wanafunzi wengi zaidi.
Ujenzi wa majengo hayo mapya utakiwezesha chuo hicho kudahili hadi Wanafunzi 800 kutoka 400 idadi iliyopo hivi sasa.
Akiwa chuoni hapo Dkt. Mpango ameeleza kuridhishwa na ujenzi.unaoendelea, kwa kuwa umezingatia matumizi bora ya nishati mbadala na nafuu na pia uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema mradi huo wa ujenzi wa majengo ya kisasa katika chuo cha ualimu cha Kabanga utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 11 hadi kukamilika kwake.
Naye Balozi wa Canada nchini Pamela O’dennel amesema ujenzi unaoendelea chuoni hapo ni wa kisasa na ni moja ya jitihada za Serikali za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.