Tutoe maoni yatakayomaliza tatizo la umaskini, ajira

0
235

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema umaskini pamoja na ukosefu wa ajira kwa vijana wengi wa Tanzania ni changamoto kuu zilizoshindwa kutatuliwa kikamilifu kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa inayomalizika mwaka 2025/2026.

Prof. Mkumbo amezungumza hayo leo Jumamosi Agosti 3, 2024 kwenye ukumbi wa Eden Highland jijini Mbeya wakati wa Kongamano la Kikanda, Kanda ya Kusini ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukusanya maoni ya wananchi katika uandishi wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 – 2050.

“Mafanikio ni mengi yaliyotokana na Dira ya Taifa ya 2025 lakini changamoto zipozipo kwani ukuaji wa uchumi haukukua kwa kiwango ambacho kingefanikisha kuondoa umaskini. Umaskini bado tunao lakini umepungua,” amesema Prof. Kitila.

Waziri huyo wa Mipango na Uwekezaji amesisitiza wananchi wa mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe na Njombe kutoa maoni yao kikamilifu hasa kwa kuzingatia changamoto za umaskini na ukosefu wa ajira ili kusaidia kupata dira itakayokuja na suluhu ya changamoto za kiuchumi zenye kuondoa umaskini na kuzalisha ajira nyingi zaidi kwa vijana.

Kufanyika kwa kongamano hili jijini Mbeya ni mwendelezo wa programu maalumu inayosimamiwa na Wizara ya Uwekezaji na Mipango ya kusikiliza wananchi, viongozi wastaafu na waliopo madarakani pamoja na makundi mbalimbali ili kupata maoni yao yatakayojumuishwa kwenye uandishi wa Dira ya Maendeleo itakayotutoa kuanzia mwaka kesho 2025 hadi 2050.