Simba pambaneni, uwezo wa kubeba kombe mnao

0
496

Tafakuri Angavu hii leo inaangazia juu ya Mnyama, Timu ya Simba SC, ambayo ni moja ya vilabu vinavyoheshimika sana barani Afrika, inayoshiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup) msimu huu na hii leo ipo ugenini nchini Algeria kukipiga dhidi ya CS Constantine baada kujipatia pointi tatu nyumbani kwa kuikanda timu ya FC Bravos do Maquis inayotokea Mji wa Luena, katika mkoa wa Moxico, Angola, goli 1-0.

Wekundu wa Msimbazi, vijana kutoka Kariakoo Jijini Dar es Salaam, Tanzania wamekuwa wakionesha uwezo wa hali ya juu katika mashindano ya kimataifa, na ushiriki wao wa mara kwa mara katika michuano ya CAF, mbali ya kuwapa uzoefu mkubwa, ni ushahidi wa ukuaji wao katika soka barani Afrika.

Tafakuri Angavu inakukumbusha tu kuwa timu ya Simba SC ni klabu yenye historia ndefu na mafanikio makubwa katika soka la Tanzania na imefanikiwa kushiriki mara nyingi katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) na Kombe la Shirikisho Afrika.

Ikumbukwe kuwa mafanikio yao makubwa ni kufikia hatua ya robo fainali na nusu fainali katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika miaka ya hivi karibuni na hakuna shaka kwa msimu huu timu hii inaweza kabisa kuleta kombe la mashindano hayo ya pili kwa ukubwa barani Afrika hapa nyumbani.

Katika Kombe la Shirikisho Afrika, Simba SC ilionesha uwezo mkubwa msimu wa 2021/2022 kwa kufika hatua ya robo fainali, ambapo walishindwa kwa ushindani mkubwa dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini. Rekodi hii inaonesha kuwa timu ina uwezo wa kushindana na vilabu vikubwa barani Afrika.

Aidha, kwa uzoefu wao wa kimataifa na kikosi chenye ubora, mashabiki wa timu hii wana matarajio makubwa ya kuona mwaka huu Simba SC ikifika angalau hatua ya fainali ya mashindano haya. Hii itakuwa hatua kubwa kwao na kulitangaza vyema soka la Tanzania kwa ujumla.

Tafakuri Angavu inamaliza kwa kusema kwamba Simba SC inapoendelea na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, matarajio ya mashabiki wao na Watanzania kwa ujumla ni makubwa. Kwa maandalizi mazuri, usajili bora, uongozi madhubuti na benchi la ufundi, Simba SC ina nafasi nzuri ya kufika mbali na hata kutwaa taji.

Kona hii inawatakia kila la heri na ushindi katika mchezo wenu wa leo dhidi ya CS Constantine

Mungu ibariki Simba SC
Mungu ibariki Tanzania.

✍🏿Na Ezekiel Simbeye