Viongozi mbalimbali ndani na nje ya Tanzania wameendelea kutoa pole kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania wote kufuatia kifo cha Rais Dkt John Magufuli.
Miongoni mwa salamu hizo ni kutoka kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, -Boris Johnson, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Akinwumi Adesina, Rais wa Somalia, -Mohamed Farmaajo na Ubalozi China nchini Tanzania.
Nyingine ni kutoka kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi na Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo Zito Kabwe.
Katika salamu zao, viongozi hao wamesema Taifa la Tanzania limepoteza Kiongozi hodari ambaye aliwapenda na kuwajali Wananchi aliyewaongoza.
Naye Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya na aliyewahi kuwa Kiongozi wa upinzani nchini humo Raila Odinga ametuma salamu zake za rambirambi na kumtaja Rais Magufuli kuwa ni mtu aliyethubutu kufanya mambo makubwa ambayo yalishindwa kufanywa na viongozi wengi.
Amesema Rais Magufuli amekuwa rafiki yake wa muda mrefu na amekuwa mtu wake wa karibu nyakati zote ngumu alipomuhitaji.
Rais Dkt Magufuli amefariki Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.
Rais Dkt Magufuli amefariki dunia kutokana na maradhi ya moyo ambayo yamekuwa yakimsumbua kwa takribani miaka 10.