Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne wamesomewa mashtaka saba ikiwemo kuendesha genge la uhalifu, kupokea rushwa, utakatishaji wa fedha pamoja na ukiukwaji wa mamlaka ya utumishi.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali Tumaini Kweka akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Salome Mshasha, amewataja washtakiwa wengine kuwa ni Silivester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey.
Kweka amesema katika shtaka la kwanza linalowahusu washtakiwa wote inadaiwa Sabaya akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai alikiuka majukumu yake ya kiutendaji kwa makusudi na kwa nia ya kutekeleza jinai na kujipatia shilingi milioni 30.
Katika shtaka la rushwa, Februari 2021 Sabaya alishawishi na kuomba rushwa ya shilingi milioni 30 kutoka kwa Godbless Swai katika eneo la Bomang’ombe wilayani Hai pamoja na kupokea rushwa ya shilingi milioni 30 kutoka kwa Elibariki Swai kwa nia ya kuzuia taarifa za uchunguzi zinazohusiana na ukwepaji wa kodi.
Kwa upande wake wakili anayewatetea washtakiwa wote, Hellen Mahuna amedai mahakamani hapo kuwa taratibu za kuwafikisha wateja wake mahakamani hapo hazikufuatwa, na kuiomba mahakama kutenda haki kwa kufuata sheria.
Akitoa uamuzi kuhusiana na hoja hiyo, Hakimu Salome amesema hakuna kifungu cha sheria kinachoilazimisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kupata kibali toka Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwani tayari Mahakama ya Moshi ilishaandika barua katika Gereza la Kisongo ili washtakiwa hao kuletwa gereza la Karanga, Moshi.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 7 mwaka huu itakapotajwa tena, na washtakiwa wamerejeshwa katika Gereza la Karanga mjini Moshi.