Refa amvumilia Kudus licha ya kuvua fulana kutoa heshima kwa Atsu

0
122

Mohammed Kudus hakupewa kadi ya njano kama sheria za FIFA zinavyotaka baada ya kuvua fulana yake na kuonesha fulana ya ndani iliyokuwa na maneno ‘R.I.P ATSU’ ikiwa ni heshima kwa Christian Atsu, raia mwenzake wa Ghana aliyefariki kutokana na tetemeko la ardhi nchini Uturuki.

Licha ya kuwa alikiuka kanuni za mpira, Kudus hakupewa adhabu kwa kile kilichoelezwa kuwa mwamuzi wa mchezo wao kati ya Ajax dhidi ya Sparta Rotterdam aliona suala hilo ni “kubwa kuliko sheria za soka.”

Kudus alifanya hivyo kufuatia goli lake la dakika ya 84 la mpira wa kutenga, na hivyo kuiwezesha klabu hiyo kuibuka na ushindi wa magoli 4-0.

Vitendo kama hivyo kwa kawaida vinaweza kusababisha kadi ya njano, lakini mwamuzi Pol van Boekel alijizuia kwa sababu “alielewa” kwa nini Kudus alikuwa na kila sababu ya kutoa heshima kwa raia mwenzake.

Kudus aliiambia ESPN baadaye, “Hii ni kubwa kuliko sheria za mpira wa miguu, inahusu maisha na kifo.

Jumamosi ilithibitishwa kuwa winga wa zamani wa Chelsea, Newcastle na Everton, Atsu ni miongoni mwa waliopoteza maisha katika tetemeko la ardhi yaliyozikumba nchi za Uturuki na Syria.