Rais Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge kuandaa kanuni zitakazoelekeza jinsi ya kufanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa nchini.
Rais Samia ametoa agizo hilo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, baada ya kupokea maazimio ya awali kutoka kikosi kazi alichokiteua cha kufuatilia hoja zilizojitokeza katika mkutano wa Wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa uliofanyika jijini Dodoma mwezi Desemba mwaka 2021.
Amemtaka Waziri huyo wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge kushirikiana na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika pamoja na kile cha Wanasheria wa Zanzibar ili kufanikisha jambo hilo.
Baadhi ya maazimio ni pamoja na uundaji wa kanuni zitakazoelekeza jinsi ya kufanya mikutano ya siasa, rushwa na maadili katika uchaguzi, ruzuku na elimu ya uraia.
Masuala mengine ya uchaguzi na Katiba Mpya nayo yapo katika maazimio ya muda mrefu.