Jeshi la polisi nchini limewataka waumini wa dini ya Kikristo na Watanzania wote kusherehekea sikukuu ya Pasaka huku wakikumbuka bado Taifa liko katika siku 21 za maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli.
Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime amesema, Jeshi hilo halitarajii kuona sherehe na shamrashamra kama ilivyozoeleka kila inapofika sikukuu hiyo, lengo likiwa ni kuendelea kuomboleza kifo cha kiongozi huyo.
Amesema Jeshi la Polisi nchini limejipanga vizuri kuhakikisha Waumini wa dini ya Kikristo wanashiriki ibada ya Ijumaa Kuu, ibada ya mkesha wa Pasaka siku ya Jumamosi na Ibada ya Pasaka siku ya Jumapili katika mazingira ya amani, utulivu na usalama na Wananchi wengine wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
Ameziomba kamati za ulinzi na usalama katika nyumba za ibada na sehemu zingine kushirikiana na Jeshi la Polisi Nchini katika suala zima la kudumisha amani, ulinzi na usalama.
Msemaji huyo wa Jeshi la Polisi Nchini David Misime, pia amewahakikishia Watanzania wote kuwa hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari, ingawa kuna matukio machache ya kiuhalifu wa kijinai na ajali za barabarani, mambo yanayoendelea kushughulikiwa.