Mgogoro KKKT Dayosisi ya Kusini Mashariki wamalizika

0
231

Mgogoro wa waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Mashariki na Askofu wao Lucas Mbedule uliodumu kwa muda wa miaka sita umefikia tamati, baada ya Mkuu wa Kanisa hilo Askofu Fredrick Shoo kuingilia kati.

Mgogoro huo umefikia tamati baada ya Askofu Shoo kukutana na viongozi wa Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Kanisa hilo mkoani Mtwara na kusuluhisha mgogoro huo kwa muda wa siku mbili.

Askofu Shoo amewaambia waandishi wa habari kuwa, Halmashauri Kuu ya Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania pia imepokea na kuridhia ombi la kujiuzulu kwa Askofu Mbedule kama alivyoomba.

Hata hivyo amesema Askofu Mbedule ataendelea kuwa Askofu wa Dayosisi hiyo ya Kusini Mashariki ya KKKT mpaka hapo utakapofanyika mkutano mkuu wa dayosisi hiyo mwezi Julai mwaka huu ambapo atachaguliwa askofu mwingine.

Kuhusu migogoro ndani ya KKKT, Mkuu huyo wa KKKT Askofu Shoo amesema mingi inatokea pale ambapo taratibu za kiutumishi na misingi ya kanisa inakiukwa.

Amesema baadhi ya Wachungaji wa KKKT wamekuwa hawafuati taratibu za kikatiba za kuwa na mikutano, matokeo yake ni migogoro kuibuka mara kwa mara.