Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amefunga mafunzo ya siku tano ya kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya bara la Afrika yaliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mafunzo hayo Mhe. Masanja amesema “Wataalamu wa masuala ya uchunguzi wamejifunza mbinu za kuzuia uharibifu wowote unaoweza kutokea kwenye maeneo ya hifadhi katika nchi wanachama wa Mkataba wa Lusaka (Lusaka Agreement).”
Amesema mafunzo hayo yameshafanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda na Tanzania itaendelea kushiriki kama nchi mwanachama ili kuzilinda hifadhi na wakati huohuo kuendeleza utalii.
Naye, Mkurugenzi Msaidizi wa Kuzuia Ujangili, Wizara ya Maliasili na Utalii, Robert Mande amesema kuwa mafunzo hayo yataendelea kufanyika ili kutekeleza sera za Serikali za kuendeleza uhifadhi.
Kwa upande wake Mshiriki wa Mafunzo kutoka nchini Kenya, Jami Yamina amesema mafunzo hayo yametoa mbinu mbalimbali za kutumia ili kuwakamata majangili na kuzikamata mali zao na kuziwasilisha mahakamani.