Makamba : Kwenye masuala ya umeme hatutadanganya watu

0
242

Waziri wa Nishati January Makamba amesema katika masuala yanayohusu nishati ya umeme hawatatoa taarifa yoyote ya uongo kwa Wananchi hata wakipigwa mishake kwa taarifa za ukweli wapo tayari.

Makamba amesema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Taarifa ya shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa mwaka 2021/2022 na uzinduzi wa mpango mkakati wa miaka 10 wa shirika hilo utakaoanza kutekelezwa kuanzia mwaka wa fedha wa 2024/2025.

“Acha tupigwe mishale, tuzongwezongwe, lakini ili tuwe huru tufanye kazi hii tukiwa tumelala usingizi hatuwezi kusema kwamba kuna mgao wakati umekaribia, hatuwezi kutoa sababu za uongo kuhusu changamoto, tutasema ukweli kwa sababu nchi hii ni yetu wote,” amesema Waziri Makamba.

Amesema hawaogopi hukumu kwa mambo ambayo changamoto zake zinajulikana na utatuzi wake unafanyiwa kazi.

“Wakati tunataka kujaza maji bwawa la Julius Nyeyere ilitoka ahadi Bungeni kwamba tungejaza Novemba 2021 na mimi nilivyosema haitowezekana nikawa adui namba moja anayehujumu mradi, kwa sababu hatukuwa tayari na ingefika siku hiyo isingewezekana, lakini tumejaza kwa wakati ambao tulikuwa tayari,” ameongeza Makamba.