Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kazi nzuri na mikakati inayofanya katika utekelezaji wa miradi ya Maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Rais ametoa pongezi hizo mkoani Dar es Salaam wakati akihitimisha maadhimisho ya wiki ya maji Kitaifa.
Pia amewahimiza Watanzania wote kuvitunza na kuvirudisha vyanzo vya maji, ili kutatua kero ya maji kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Wakati huo huo Rais Samia Suluhu Hassan amezindua programu wezeshi ya simu (Mobile App) iitwayo Maji App, inayopatikana katika gulio la Google (Google Play store).
Programu hiyo itazirahisishia mamlaka husika kuona makusanyo, mauzo na idadi ya miradi ambapo kwa Wanannchi watanufaika kuona kiwango cha matumizi yao ya maji ‘Units’ na taarifa za mamlaka za Maji kwa kutumia simu zao za mkononi.
Rais Samia amehimiza programu hiyo wezeshi kupakiwa taarifa mbalimbali kwa wakati, na kutolea mfano wa baadhi ya mitandao ya interneti ya Serikali kutopandishwa taarifa zao kwa wakati.
“Natarajia App hii itawasaidia Wananchi na taarifa zitapandishwa kwa wakati, sio kama wengine ukifungua vitu vyao utakuta taarifa zile zile tatu za siku zote.” ameelekeza Rais Samia
Kwa upande wake Waziri wa Maji Jumaa Aweso ametoa tathmini ya miradi 126 ya maji ambayo ilikuwa kero kwa Wananchi lakini sasa kero hiyo imetatuliwa kwa kuweka Wakandarasi wapya waliofanikisha miradi hiyo kuanza kufanya kazi.
“Nimezunguka majimbo yote nchi nzima kufuatilia miradi ya maji kichefuchefu na kuifanyia ufumbuzi, tunakwenda kuzindua miradi ya maji 1,176 vijijini na miradi ya maji 111 mijini, tunakwenda kununua mitambo 25 ya maji kila mkoa kutakuwa na mtambo wake wa maji.’ amesema Waziri Aweso