Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) mkoa wa Kilimanjaro, Grace Kihwelu amesema anajisikia amani kusimama mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na jitihada zinazoendelea za kujenga umoja wa Kitaifa.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Wanawake wa CHADEMA yaliyoandaliwa na BAWACHA, Kihwelu ambaye pia amewahi kuwa Mbunge wa viti maalum kupitia CHADEMA amesema anafarijika kuona Rais Samia Suluhu Hassan akiwa ameketi na mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe na kwamba hiyo ndio maana halisi ya umoja kwa Watanzania.
Mwenyekiti huyo ameelezea namna ambavyo wao kama BAWACHA wameanza kuchukua hatua mbalimbali za kusaidiana na jamii kurejesha uoto wa asili kwenye maeneo ya mkoa huo, ili kupunguza athari za mabadiliko ya Tabianchi.
Kihwelu amempongeza Rais Samia kwa namna alivyoshirikiana na Mwenyekiti wao Mbowe kurejesha uhusiana na upendo miongoni mwa Watanzania na sasa Taifa limekuwa na mshikamano baina ya viongozi na Wananchi.