Kwa mara ya kwanza Ikulu ya Marekani (White House) imepata raia wa nchi hiyo mwenye asili ya Afrika kuwa msemaji wake baada ya Rais Joe Biden wa nchi hiyo kumteua Karine Jean-Pierre (44) kushika wadhifa huo.
Rais Biden amesifu utendaji kazi wa Jean-Pierre na kusema amekuwa akimuheshimu kwa kipindi kirefu.
“Karine sio tu analeta uzoefu, talanta na uadilifu unaohitajika kwa kazi hii ngumu, lakini ataendelea kuongoza njia kwenye mawasiliano ya kazi ya utawala wa Biden – Harris kwa niaba ya watu wa Marekani.”amesisitiza Biden
Jean-Pierre ataanza kazi wiki ijayo akichukua nafasi ya Jen Psaki.
“Nangoja kwa hamu kuona ukileta mtindo na upekee kwenye hii kazi.” amesema Psaki wakati akitoa taarifa hiyo
Kwa upande wa Jean-Pierre amesema ataifanya kazi hiyo ya Msemaji wa Ikulu wa Marekani kwa moyo na kuongeza kuwa ni heshima na fursa nzuri kwake kutekeleza jukumu hiyo.