Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza nafasi za kujiunga na jeshi kwa vijana ambao wametumikia au wamefanya mafunzo ya kujitolea katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa muda wa miaka miwili, kisha wakarejeshwa majumbani.
Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ Luteni Kanali Gaudentius Ilonda amesema, vijana hao ni wale ambao walifanya mafunzo JKT na walipotimiza miaka miwili wakapewa vyeti baada ya kukosa fursa aidha kuandikishwa JWTZ au katika taasisi ama vyombo vingine vya ulinzi na usalama na hivyo kurejeshwa majumbani
Amesema kijana atakayepata nafasi ya kujiunga na jeshi anatakiwa awe ni raia wa Tanzania wa kuzaliwa, awe na umri wa miaka 18 hadi 26 kwa waliohitimu kidato cha nne hadi cha sita na kwa wenye elimu ya juu kufikia shahada ya uzamili wawe na umri usiozidi miaka 27.
Kigezo kingine awe kijana ambaye hajawahi kupatikana na kosa la kijinai au kushtakiwa mahakamani na kufungwa.
Awe pia hajawahi kutumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo na awe na cheti cha kuhudumia JKT kwa muda wa miaka miwili.