Jeshi la polisi mkoani Tanga limeokoa zaidi ya shilingi milioni themanini kutoka kwenye nyara za serikali zilizokua zikisafirishwa wilayani Handeni.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga Safia Jongo, amesema kukamatwa kwa nyara hizo kumetokana na operesheni endelevu inayofanywa na jeshi la polisi mkoani humo ya kutokomeza vitendo vya uhalifu.
“Hatutamvumilia mtu au kikundi chochote kilichojipanga kutuharibia sifa ya mkoa wetu ambao kwa historia Tanga ni mkoa wa watu wastaarabu. Tunataka kuendelea kubaki na sifa hiyo tukiwa salama na wenye amani na katika hili nitasimama imara,”-amesema Kamanda Safia.
Nyara zilizokamatwa ni pamoja na meno ya tembo na nyama za porini za swala pamoja na twiga.
Katika hatua nyingine jeshi hilo limekamata magobore sita yanayotengenezwa kienyeji wilayani handeni na tayari watu kumi na wawili wanashikiliwa na jeshi hilo wakisubiri taratibu za kisheria zikamilike kabla ya kufikishwa mahakamani.