Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango amewataka baadhi ya viongozi wanaochangia katika uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji kuacha mara moja ili kunusuru Taifa dhidi ya athari za uharibifu zinazojitokeza hivi sasa.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Wahariri na Wadau wa Uhifadhi Mazingira na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji linalofanyika katika Ukumbi wa Masiti mkoani Iringa ambapo amesisitiza kuwa ni lazima kushirikiana na kuwa na jitihada za pamoja baina ya serikali, dini, sekta binafsi, vyombo vya Habari pamoja na vyama vya siasa katika kupambana na uharibifu wa Mazingira nchini.
Halikadhalika amewaasa Waandishi wa Habari kuendelea kutumia ushawishi walionao katika jamii kuihamasisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira na kuziagiza taasisi za Serikali kuhakikisha zinawashirikisha Waandishi wa Habari na Vyama mbalimbali vya Wanahabari vinavyojitoa kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira.
Pamoja na kutetea maslahi ya taifa Dkt.Mpango amewataka waandishi kujiepusha na kupokea fedha, mali au vishawishi vingine Kutoka kwa watu wachache wenye jeuri ya pesa au madaraka ili kupindisha ukweli wa mambo kinyume na maslahi ya taifa au wananchi wengi wanyonge wasio na sauti.
Makamu wa Rais amewasihi kutumia Kongamano hilo kufanya mijadala ya kina ya kujenga na kupata maazimio ambayo pamoja na mambo mengine, yatajumuisha hatua mbalimbali zitakazochukuliwa katika kuongeza juhudi za kuhabarisha umma kuhusu utunzaji na ulinzi wa mazingira hususan katika Vyanzo vya Maji.