Bunge lapitisha azimio kumpongeza Rais

0
132

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeazima kwa kauli moja kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kupata tuzo ya Mjenzi Mahiri kwa mwaka 2022 iliyotolewa huko Accra, Ghana na Benki ya Maendeleo ya Afrika(AfDB), akiwa ni Rais wa 12 kupata tuzo hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 2016.

Azimio hilo liliwasilishwa bungeni jijini Dodoma na Mbunge wa viti maalum Zainabu Katimba ambaye amesema tuzo hiyo imetolewa kwa kutambua mchango wa Rais Samia kama mwanamke mzalendo na Rais wa kwanza wa Tanzania kupata tuzo hiyo akiwa anaongoza serikali ya awamu ya sita kwa mafanikio makubwa katika kuendeleza sekta ya miundombinu ya usafirishaji hususani eneo la barabara.

Sababu nyingine ni juhudi kubwa anazofanya kuendeleza miundombinu ya usafirishaji ikiwemo kusimamia na kufungua miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara na reli hapa nchini.

Pia amesema Rais Samia Suluhu Hassan anapaswa kupongezwa kufuatia kutambuliwa kwake kuwa miongoni mwa viongozi 100 wenye ushawishi mkubwa duniani, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na gazeti la Time la nchini Marekani na kuchapishwa tarehe 24 mwezi huu.

Wakichangia azimio hilo, baadhi ya wabunge wamesema Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi kifupi alichokaa madarakani amefanya mambo makubwa, hivyo anastahili pongezi.