Yanga yaomba kubadilishiwa ratiba dhidi ya Singida BS

0
640

Yanga SC imetuma maombi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) kuhusu kuangaliwa upya kwa ratiba ya michezo yao dhidi ya Singida Big Stars.

Kwa mujibu wa ratiba, Yanga ina michezo miwili na Singida BS ambapo mchezo wa ligi ni Mei 4 na Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ni Mei 7 huku pia ikitakiwa kucheza mchezo wa Nusu Fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika Mei 10 mwaka huu.

Kutokana na ufinyu huo wa muda, Rais wa Yanga Mhandisi Hersi Said amesema “mcheza kwao hutunzwa,” hivyo wanaamini kwamba mamlaka hizo zitawasaidia ili wapate muda wa kutosha kujiandaa na mchezo huo mkubwa na muhimu si tu kwa Yanga, bali kwa Taifa.

“Hiyo ndio karata yetu muhimu ya hapa nyumbani,” amesema Hersi akisisitiza kuwa endapo ratiba itabaki kama ilivyo wakimaliza mchezo wa pili dhidi ya Singida, watarejea Dar es Salaam Mei 8, hivyo watakuwa na siku moja tu, ambayo hawajui kama watapumzika au watajiandaa na mchezo wao dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini.

Yanga ipo kwenye safari ya kuwania kutwaa makombe manne msimu huu, ikiwa tayari imeshinda ngao ya jamii, huku mwelekeo wao ukiwa kwenye ligi na kombe la shirikisho Tanzania na Afrika.