Yanga SC inatarajia kuondoka nchini kesho alfajiri kuelekea Nigeria kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rivers United.
Afisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema msafara huo utakuwa na watu 49 wakiwemo wachezaji, viongozi wa klabu na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania.
Aidha, amesema wanatambua kwamba Rivers United huwa bora sana inapotumia uwanja wake wa nyumbani, lakini wao wamejiandaa vizuri zaidi kwani wanatambua umuhimu wa mchezo huo, na hivyo watahakikisha wanapata matokeo mazuri, ili kupunguza mzigo kwenye mechi ya marudiano.
“Sisi Young Africans hatutamani kufikia kufanya ‘comeback’ ya goli tano hapa… Wakiwa kwao wale mabwana ni watu tofauti kabisa, ni timu ngumu, timu tishio,” amesema Kamwe.
Mbali na kwamba wachezaji wanaendelea kujiandaa vya kutosha, Kamwe amewataka mashabiki kusimama katika nafasi yao ikiwa ni pamoja kuiombea timu na kujitokeza uwanjani kwa wingi.
Mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano utapigwa Aprili 23 na marudiano utachezwa Aprili 30 mkoani Dar es Salaam.