Yanga kunogesha sherehe za Uhuru wa Malawi

0
454

Serikali ya Malawi imeialika Yanga SC kutoa burudani katika maadhimisho ya miaka 59 ya uhuru wa Taifa hilo, sherehe itakayofanyika Julai 6 mwaka huu ambapo watacheza dhidi ya Nyasa Big Bullets FC.

Taarifa hiyo imetolewa leo na Afisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kueleza kwamba ratiba hiyo haikuwepo kwenye mipango yao lakini watakwenda.

“Kwa heshima ambayo Serikali ya Malawi imetupatia Young Africans, kuona kwamba tunatosha kwenda kutoa burudani kwa Wamalawi wakiwa wanaadhimisha sherehe zao za uhuru, uongozi wa Young Africans ukapiga simu kwa wachezaji kuwaambia kwamba tunatakiwa kwenda Malawi,” amesema Kamwe.

Amewapongeza wachezaji wao kwa kuitikia wito huo licha kwamba walikuwa mapumzikoni na kwamba wataondoka nchini Julai 5 mwaka huu wakiwa na wachezaji 15 wa kikosi cha kwanza pamoja na wachezaji wengine wa nyongeza kutoka kikosi cha vijana.

Ali Kamwe ameongeza kuwa wanawahi ili Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye naye amealikwa kwenye sherehe hizo atakapofika, aikute timu yake imefika, na wampokee.