Timu ya Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ulinzi na Mambo ya Ndani, imepokea mpango mkakati wa pamoja wa jinsi ya kuendeleza michezo nchini na mpango mkakati wa muda mfupi wa kuandaa timu za Taifa kushinda kwenye mashindano ya kimataifa ikiwa ni pamoja na jumuiya ya madola yatakayofanyika nchini Uingereza Julai 2022.
Mipango hiyo imewasilishwa na kamati maalum inayojumuisha Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo (WUSM), Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT)iliyoundwa kufuatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka vyombo hivyo vya Michezo kuchukua hatua za kuimarisha Michezo ili kuleta mafanikio kwenye mashindano ya kitaifa na kimataifa.
Ikiwasilisha taarifa hiyo ya mipango Kamati hiyo ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Baraza la Michezo linalojumuisha vyombo mbalimbali vya dola nchini ilieleza kuwa mipango hiyo imekuja na mkakati mahususi ili kutumia vipaji vilivyoko katika vyombo hivyo kusaidia Timu mbalimbali za Taifa.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini Yusuph Singo, amesema vijana wengi walioko kwenye majeshi nchini wanavipaji ambavyo bila kuweka mikakati hawatapata nafasi ya kuisaidia nchi.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya kuandaa Mpango Mkakati wa pamoja wa WUSM, BMT na BAMMATA, Kanali Erasmus Bwegoge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Michezo Kanda ya JKT, amesema mkakati wa mipango hiyo imepambanua kikamilifu malengo, majukumu, mikakati, shabaha, na viashiria vya mafanikio na umetoa mwelekeo wa hatua mbalimbali zitakazochukuliwa na wadau wote ili kufikia lengo la Mhe. Rais la kufanya vizuri katika Michezo kimataifa.