Wagonga nyundo wa jiji la London, – West Ham United wamepata ushindi wa kwanza kwenye ligi ya England msimu huu, wakiwa chini ya kocha Manuel Pellegrini baada ya kuitandika Everton mabao matatu kwa moja kwenye dimba la Goodison Park.
Myukraine, – Andriy Yarmolenko aliifungia West Ham mabao mawili katika dakika za 11 na 31 kabla ya Marco Arnautovic kupigilia msumari wa mwisho katika dakika ya 61, huku bao pekee la kufutia machozi kwa Everton likifungwa na Gylfi Sigurdsson katika dakika ya 45.
Ushindi huo unamaliza ukame wa West Ham kucheza michezo Minne mfululizo bila kupata ushindi, na endapo wangepoteza mchezo huo wangeweka rekodi ya kuwa na mwanzo mbaya zaidi wa msimu katika klabu hiyo.
Katika matokeo mengine ya mchezo wa ligi ya England uliochezwa Septemba 16, Wolverhampton Wenderers wakiwa nyumbani wameibuka na ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya Burnley na leo Septemba 17 utachezwa mchezo mmoja ambapo Southampton watakuwa nyumbani kwenye dimba la ST. Marys kuwakaribisha Brighton & Hove Albion.