Waziri Mkuu aagiza kurejeshwa kwa michezo ya SHIMIWI

0
540

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza wizara zote zinazohusika na uratibu na uandaaji  wa Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) wahakikishe wanakutana na kuweka mpango wa kurejesha michezo hiyo ili watumishi wa umma wapate fursa ya kushiriki na kujikinga na maradhi yasiyoambukiza.   
 
Amesema michezo hiyo ya SHIMIWI ni muhimu kwa sababu ilikuwa inawakutanisha Watumishi wa Wizara za Serikali na Taasisi zake na ilisaidia sana kuboresha afya zao na kuongeza hamasa ya utendaji kazi hivyo kuongeza tija na ufanisi wa kazi.
 
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo wakati alipomuwakilisha Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wakati wa mbio za hisani za “CRDB Bank Marathon” zilizofanyika katika viwanja vya The Greens, Oysterbay  Dar es Salaam.
 
Waziri Mkuu amesema mashindano hayo ya SHIMIWI yaliwasaidia watumishi wa umma kupambana na magonjwa sugu yasiyoambukiza tofauti na sasa.

“Nakumbuka mara ya mwisho michezo hii ilifanyika mwaka 2014.”

“…Naelekeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jinsia, Wazee na Watoto  na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kuweka mikakati ya pamoja ya kufufua michezo na ushiriki wa michezo kwa watumishi, wanafunzi na wananchi kwa ujumla.”
 
Kadhalika, Waziri Mkuu ameiagiza TAMISEMI ihakikisheni inasimamia kwa ukaribu ushiriki wa michezo kwa watumishi na wananchi, pia michezo kama vile jogging, marathon, mchakamchaka nayo inatakiwa ipewe kipaumbele hususan kwa wanafunzi.