Wamiliki wa Seattle Sounder kuinua michezo Tanzania

0
3845

Kampuni ya kimataifa ya Vulcan Inc. kupitia kampuni yake tanzu ya Vulcan Arts and Intertainment imeeleza utayari wake wa kusaidiana na serikali ya Tanzania katika kuinua sanaa na michezo.

Hayo yameelezwa na mkurugenzi mwandamizi wa masoko na ubia wa kampuni ya Vulcan Inc. Luke Grothkopp, wakati wa mazungumzo yake na
ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu wa wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, mazungumzo yaliyofanyika mjini Seattle.

Grothkopp amesema kampuni hiyo ilitaka kuwekeza Tanzania miaka 10 iliyopita, lakini kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wao ubia huo haukuendelea.

“Mwanzilishi wa kampuni hizi ambaye sasa ni marehemu Bw. Allen, alifika Tanzania na alikuwa mtu wa masuala ya sayansi na uhifadhi wa mazingira na alipenda kufanya kazi na Tanzania lakini haikuwezekana, leo sisi tuko tayari kuyaendeleza mawazo yake hayo kwa kuingia ubia wa kusaidia michezo na sanaa nchini Tanzania,” amesema Grothkopp

Pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kushiriki filamu ya The Royal Tour akisema ni filamu ambayo imeongeza chachu ya kuwajulisha Wamarekani na watu wengine duniani uzuri wa Tanzania katika utalii na uwekezaji.

Naye Dkt. Abbasi ameikaribisha kampuni hiyo ya Vulcan Inc. kushirikiana na Tanzania kwani ni nchi iliyosheheni vipaji vya michezo na sanaa na kuwaahidi ushirikiano kutoka kwa wadau wote muhimu.

Kampuni ya Vulcan yenye makao makuu yake mjini Seattle nchini Marekani, tayari imewekeza mabilioni ya dola katika sekta za michezo na sanaa ikiwemo kumiliki timu ya mpira wa miguu ya Seattle Sounders
inayofanya vizuri katika Ligi Kuu ya Soka ya Marekani,
klabu ya michezo ya Sea Hawks, klabu ya mpira wa kikapu ya Portland Trailblazers inayoshiriki NBA na viwanja vya michezo zaidi ya 20.

Pia inamiliki vituo kadhaa vya makumbusho ikiwemo makumbusho kubwa ya sanaa na historia ya utamaduni wa Hip Hop.