Chama Waandishi wa Habari nchini Ghana kimelaani tukio la mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi nchini humo – Ahmed Hussein-Suale aliyeuawa kwa kupigwa risasi mara tatu siku ya Januari 16.
Tukio hilo linafuatia ripoti kadhaa za kiuchunguzi alizozifanya Hussein-Suale akiwa chini ya kampuni ya Tiger Eye Private Investigations ambapo alihusika katika kufichua vitendo vya rushwa kwenye soka la Ghana na ripoti hizo zilisababisha aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Ghana – Kwesi Nyantakyi kufungiwa maisha kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu.
Rais wa Chama cha Wanahabari nchini Ghana – Roland Affail Monney amesema Hussein-Suale alikuwa shujaa wa taifa hilo aliyetumia kalamu yake kuua uovu na sio kuua watu kwa risasi kama alivyouawa yeye hivyo tukio hilo limeijeruhi tasnia ya habari nchini Ghana.
Muda mchache baada ya kuonyeshwa kwa makala walizotengeneza wakina Hussein-Suale, Mbunge Kennedy Agyapong alisambaza picha za Hussein-Suale kupitia vyombo vya habari akitaka mwandishi huyo wa habari aadhibiwe vikali kwa kuwachafua watu mashuhuri nchini humo.
Hata hivyo mbunge huyo amekana kuhusika kwa namna yoyote na mauaji hayo akisema shutma zinazoelekezwa kwake si za kweli.
Mourinho ateetea kufanya vibaya akiwa na Manchester United
Aliyekuwa kocha wa Manchester United ya England – jose Mourinho ametetea mwenendo mbovu wa timu hiyo ilipokuwa nanye ambao ulipelekea kufukuzwa kazi kwenye timu hiyo mwezi Desemba mwaka jana.
Mourinho amesema watu hawajui kinachotokea nyuma ya pazia ndiyo maana wanakosoa kirahisi matokeo ya kinachofanyika nyuma ya pazia.
Kocha huyo Mreno anasema mambo hayakuwa shwari ndani ya Manchester United ndiyo mana alivurunda kwenye msimu wake wa mwisho hali iliyosababishwa na kutoungwa mkono na bodi ya klabu hiyo.
Anasema kuna maamuzi alikuwa anataka yachukuliwe ili timu ikae sawa lakini bodi haikuonyesha ushirikiano jambao lililopelekea mpasuko kwenye timu na kuifanya ikose matokeo mazuri.
Kati ya mambo ambayo Mourinho amewahi kuyalalamikia hadharani alipokuwa akiwanoa Mashetani Wekundu ni pamoja na uongozi kushindwa kukamilisha usajili wa wachezaji aliokuwa anawataka huku yeye pia akilalamikiwa kwa kutokuelewana na wachezaji wake wakiongozwa na Paul Pogba.
Hata hivyo Mourinho ameongeza kuwa hafikirii kustaafu kufundisha kabumbu kwani umri wake bado mdogo na siku si nyingi atarejea kufundisha kandanda kwenye timu kubwa.