Vettel akiri adui yake ni yeye mwenyewe

0
2358

Dereva wa kampuni ya Ferari,- Sebastian Vettel amesema kuwa adui yake mkubwa katika kinyang’anyiro cha kuwania taji la mbio za langalanga msimu huu baina yake na dereva wa Marcedes, – Lewis Hamilton ni yeye mwenyewe.

Vettel ambaye yupo alama 30 nyuma ya mpinzani wake Hamilton, amefanya makosa kadhaa msimu huu yaliyotoa faida kubwa kwa Marcedes na amesema bado ana nafasi ya kufanya vema kutokana na ubora wa kampuni ya Ferari inayoongoza kwa kuwa gari lenye kasi zaidi kwenye mbio za langalanga kulinganisha na Marcedes.

Mjerumani huyo amesema kuwa wapo kwenye nafasi nzuri ya kushinda na adui yao mkubwa ni wao wenyewe kama kampuni na si mtu mmoja kama watu wanavyofikiri na kinachohitajika ni umakini wakati wote wa mchezo ili kuepuka makosa yatakayotoa nafasi kwa wapinzani kushinda kama ilivyokuwa kwenye mashindano kadhaa yaliyopita.

Kwa upande wake bingwa mtetezi wa mbio za langalanga, Lewis Hamilton amesema kuwa ufundi wa kwenye usukani ndiyo utadhihirisha nani ni mkali na si maneno ya nje na kuongeza kuwa bado kuna alama nyingi kuelekea kwenye ubingwa.

Vettel na Hamilton ni wapinzani wakubwa kwenye mbio za langalanga na Vettel alianza vema msimu huu kabla ya Hamilton kuzinduka katika mashidano Matano yaliyopita ambapo ameshinda matatu na sasa kila mmoja anapambana kushinda mashindano yanayofuata ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kushinda taji la dunia.