Mchengerwa kwenye vilabu vya Uingereza

0
210

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa ametembelea miundombinu ya michezo nchini Uingereza na kufanya mazungumzo na wamiliki wake lengo likiwa ni kuboresha miundombinu ya michezo nchini.

Katika ziara hiyo Mchengerwa ametembelea kiwanja cha King Power kinachomilikiwa na klabu ya Leicester City na St Mary’s kinachomilikiwa na klabu ya Southampton na kujionea miundombinu mbalimbali ya michezo na kujifunza namna bora ya kuiendeleza na usimamizi wa miundombinu hiyo.

“Tumejifunza mambo mambo mengi makubwa ambayo sisi pia tunaweza kuyaiga na kuyaboresha kutoka kwa wenzetu hawa ambao wamepiga hatua kubwa kwenye anga ya michezo na sisi tukapiga hatua ya haraka” amesema Mchengerwa

Akiwa kwenye ziara hiyo Mchengerwa alipata fursa ya kushuhudia fainali za kombe la ngao ya jamii mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa King Power katika mji wa Leicester baina ya timu ya Liverpool na Manchester City ambapo Liverpool imeibuka mshindi wa kombe hilo kwa kuibamiza Manchester City Magoli matatu kwa nunge.

Mara baada ya kutembelea miundombinu hiyo, Mchengerwa ameelezea kuwa Tanzania inakwenda kufanya mapinduzi makubwa kwenye michezo kwa kuimarisha miundombinu yake ili kuwa na maeneo ambayo yatazalisha wachezaji wengi ambao watakuwa kwenye kiwango cha kimataifa.

Mchengerwa amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuona kuwa michezo inakua kwa kasi kubwa na kutoa ajira kwa watanzania wengi lengo likiwa ni kuchangia kwenye uchumi wa taifa kwa ujumla.