Shirikisho Soka Nchini (TFF) limesema kuwa tiketi za mchezo baina ya watani wa jadi Simba na Yanga utakaopigwa Septemba 30 mwaka huu, zitaanza kuuzwa mapema ambapo kiingilio cha juu kwenye mtanange huo kikiwa ni Shilingi elfu 30 na cha chini kikiwa ni Shilingi elfu Saba.
Msemaji wa TFF Clifford Ndimbo amesema kuwa tiketi za mchezo huo utakaopigwa kwenye nyasi za dimba la Taifa jijini Dar es salaam zitaanza kuuzwa Septemba 20 huku kukiwa na taratibu mbalimbali za kuingia uwanjani zitakazosaidia kupunguza matatizo yanayoweza kujitokeza.
Watani wa jadi Simba na Yanga watakutana kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2018/2019, ambapo mara ya mwisho zilipokutana kwenye Ligi Kuu Yanga iliambulia kipigo cha bao moja kwa bila.