TFF: Hatukualika wageni mkutano wa CAF

0
259

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawaomba wadau kupuuza taarifa potofu zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii kuhusu mialiko ya Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) uliofanyika jana nchini Tanzania.

Mkutano huo wa 44 wa CAF uliofanyika jijini Arusha uliandaliwa na Shirikisho hilo, na TFF ilikuwa mwenyeji.

Wajumbe wa Mkutano huo wametajwa katika Katiba ya CAF, na waalikwa wengine nao wanaalikwa na Shirikisho hilo na si TFF kama inavyopotoshwa.

Nafasi ya TFF ilikuwa ni kutafuta mgeni rasmi wa kufungua Mkutano huo, si vinginevyo.

Ukiondoa Kamati ya Ndani ya Maandalizi (LOC), washiriki wengine wote walialikwa na CAF yenyewe.