Taifa Stars uso kwa uso na Cape Verde

0
2379

Timu ya Taifa ya mpira wa miguu – Taifa Stars jioni ya leo inateremka dimbani huko mjini Praia kuikabili Cape Verde katika mchezo wa tatu wa hatua ya makundi ya kuwania tiketi ya kufuzu kwa fainali za kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwaka 2019 nchini Cameroon.

Kuelekea mchezo huo,  kocha mkuu wa Taifa Stars, -Emmanuel Amunike amesema kuwa kikosi chake kipo tayari kuwapa furaha watanzania katika mchezo huo dhidi ya wenyeji Cape Verde.

Amunike amesema kuwa huu ni wakati wa wachezaji wake kufanya jambo jema kwa nchi yao kwa kupata ushindi na kutengeneza njia ya kufuzu kwa fainali za AFCON kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980 huku Mkurugenzi wa Michezo kutoka wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Yusuph Singo akisema kuwa wachezaji wapo tayari kwa mchezo huo.

Taifa Stars inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi lake la L nyuma ya vinara Uganda wenye alama Nne, huku Lesotho wakiwa katika nafasi ya pili wakiwa na alama mbili sawa na Stars na Cape Verde inaburuza mkia.