Timu ya Taifa ya soka – Taifa Stars leo inacheza mchezo muhimu wa kuwania kufuzu kwa michuano ya mataifa ya Afrika (AFCON 2019) dhidi ya timu ya taifa ya Cape Verde ambayo walicheza nayo Ijumaa iliyopita na kuambulia kichapo cha mabao matatu kwa sifuri.
Mchezo wa leo dhidi ya Cape Verde ndio utakaoamua mustakabali wa Taifa Stars kucheza michuano ijayo ya mataifa ya Afrika hasa baada ya kupoteza mchezo uliopita mjini Praia.
Ili Kuendelea kuwa na matumaini ya kushiriki michuano hiyo mwaka 2019, Taifa Stars inalazimika kushinda mchezo dhidi ya Cape Verde na kufikisha alama tano ambazo zitaiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kwa michuano hiyo nchini Cameroon.
Ili kuongeza nguvu kwenye mchezo wa leo, kocha wa Stars Emmanuel Amunike amemuita mchezaji kiraka wa timu ya Simba,- Erasto Nyoni ambaye ni moja ya wachezaji wazoefu na waliocheza kwa muda mrefu kwenye timu ya Taifa ya Tanzania.
Stars itawakosa wachezaji wake wawili ambao ni mlinzi wa kulia Hassan Kessy Ramadhan na Thomas Ulimwengu ambao wote wanatumikia adhabu ya kuwa na kadi mbili za njano.
Kwenye kundi la L ambalo Taifa Stars ipo, Uganda inaongoza ikiwa na alama saba ikifuatiwa na Cape Verde yenye pointi nne huku Taifa Stars na Lesotho zikiwa na alama mbili kila mmoja na zote hazijashinda mchezo wowote hadi sasa.