Spurs kuikabili Leipizig, Valencia kutoana jasho na Atlanta
Kivumbi cha michezo ya marudiano ya hatua ya mtoano ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya kinatimka usiku wa leo kwa michezo miwili.
Tottenham Hotspurs inayonolewa na Jose Mourinho itakuwa nchini Ujerumani kumenyana na RB Leipizig katika mchezo ambao Spurs wanahitaji ushindi kwa udi na uvumba.
Leipizig wao wanahitaji sare tu kutinga robo fainali baada ya kupata ushindi wa bao moja kwa bila katika mchezo wa kwanza wakiwa ugenini mjini London, huku pia wakipewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo wa usiku wa leo.
Nchini Hispania, Valencia wana mlima mkubwa wa kupanda mbele ya Atlanta ya Italia baada ya kukubali kichapo cha mabao manne kwa moja katika mchezo wa kwanza kwenye dimba la San Siro.
Atlanta wanahitaji sare tu au kufungwa mabao yasiyozidi mawili ili kutinga robo fainali huku Valencia wakitakiwa kushinda kuanzia mabao matatu kwa bila kama wanataka kusonga mbele.
Hapo kesho majogoo wa jiji Liverpool watakuwa nyumbani kukipiga dhidi ya Atletico Madrid huku PSG wakiwaalika Borussia Dortmund katika mchezo utakaochezwa bila kuwepo Mashabiki kutokana na tishio la virusi vya corona.