Simeone aomba radhi

0
994

Kocha wa timu ya Atletico Madrid ya Hispania,- Diego Simeone amewaomba radhi wale wote waliokwazika na ushangiliaji wake wa goli la kwanza la timu yake kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Juventus Turin ya Italia.

Simeone  maarufu kama El Cholo amesema kuwa, alifanya hivyo kwa moyo wa dhati bila unafiki na kama kuna mtu anaona alikosea basi amsamehe na kukiri kuwa kitendo alichokifanya sio kizuri kwa jamii.

Kocha huyo raia wa Argentina alishangilia goli la kwanza lililofungwa na mlinzi wake wa kati Mruguay Jose Maria Gimenez kwa mtindo wa aina yake na mwenyewe amesema kuwa alishawahi kufanya hivyo wakati anacheza soka kwenye timu ya Lazio ya Italia na amefanya hivyo tena ili kuonyesha mashabiki kuwa wapo pamoja.

Katika mchezo huo,  Magoli mawili yaliyofungwa na walinzi wa kati Raia wa Uruguay, -Jose Maria Gimenez na Diego Godin yalitosha kuipa ushindi mnono timu  hiyo ya Atletico Madrid dhidi ya Juventus Turin.

Walinzi hao walifunga magoli hayo ndani ya dakika Tano kwenye dakika za 78 na 83 za mchezo huo ambao ulimrudisha kwa mara ya kwanza Cristiano Ronaldo kwenye mji mkuu wa Hispania, -Madrid tangu aachane na timu yake ya zamani ya  Real Madrid.

Pamoja na ushindi huo wa bao mbili kwa bila,  timu hiyo ya Diego Simeone ilinyimwa Penati na goli lililofungwa na Alvaro Morata lilikataliwa baada ya msaada wa video kuona halikuwa goli halali,  lakini baadae wakafunga mara mbili kupitia walinzi hao wa kati toka Amerika ya Kusini.

Wachezaji wawili wa Atletico Madrid, -Diego Costa na Thomas Partey na mlinzi wa kushoto wa Juventus, – Alex Sandro watakosa mchezo wa marudiano kutokana na kupata kadi za pili za njano kwenye mchezo huo uliochezwa Jumatano Februari 21 mwaka huu.