Ile mbiu ya shangwe za mashabiki wa Simba na Yanga katika mtandao wa Twitter imekosa mpulizaji baada ya timu hizo kulazimishana sare ya goli 1-1.
Mchezo huo uliojawa na mbwembwe, kejeli na burudani za kila namna umechezwa leo kati ya mashabiki wa Simba na mashabiki wa Yanga, ikiwa ni sehemu ya tamasha la Watanzania wanaotumia mtandao wa Twitter (TOTBonanza) lililofanyika katika viwanja vya Posta Kijitonyama.
Mchezo huo ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu huku kila timu ikijigamba kwamba itamchapa mpinzani wake. Timu hizo mbili zimeungwa mkono na vilabu vya Simba na Yanga, ambavyo vilitoa jezi kwa mashabiki kuvaa, na pia viongozi wa timu hizo wamehudhuri mchezo huo.
Yanga ndio walikuwa wa kwanza kupata goli katika kipindi cha kwanza, huku Simba ikisawazisha dakika ya 89, na hivyo mchezo kumalizika bila mbabe.
TOT Bonanza ni jukwaa ambalo hukutanisha zaidi watumiaji wa mtandao wa Twitter ambao hujumuika pamoja kwa mambo mbalimbali ikiwemo burudani na soga.
Mbali na hayo, washiriki wa bonanza hilo hushiriki kwa kuuza na kununua bidhaa mbalimbali kutoka kwa wajasiriamali ambao huleta bidhaa au kutangaza huduma wanazotoa.
Jukwaa hilo hufanyika mara tatu kwa mwaka ambapo kwa mara ya kwanza lilifanyika Desemba 2018.