Simba yafuzu robo fainali Ligi ya Mabingwa

0
191

Mabingwa wa Tanzania mara tatu mfululizo, Simba SC imetinga hatua ya Robo Fainali ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichapa mabao 4-1 AS Vita Club kutoka DR Congo na kufikisha alama 13 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote katika Kundi A.

Simba ilikuwa wa kwanza kuliona lango la wageni katika mchezo ulichezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kupitia kwa winga machachari Luis Miquissone dakika ya 30 kwa shuti kali akipokea pasi kutoka kwa Bernard Morisson.

Dakika ya 32 kiungo Zemanga Soze akasawazishia AS Vita Club na kuvunja rekodi ya Simba ya kutoruhusu bao.

Kabla ya mapumziko Simba walipata bao la pili kupitia kwa kiungo mshambuliaji Clatous Chama dakika ya 45+1 na kuipeleka Simba mapumziko ikiwa kifua mbele.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko hata hivyo Simba ilinufaika na mabadiliko hayo akitokea benchi Larry Bwalya aliipatia Simba bao la tatu akimalizia pasi ya Clatous Chama dakika ya 66.

Mnamo dakika ya 83 Clatous Chama alirudi tena kambani kwa bao safi kwa kuwachambua mabeki wa As Vita pamoja na golikipa wao mara baada ya kupokea pasi ya Luis Miquissone.

Katika mchezo mwingine wa kundi hilo vibonde Al-Merrikh ya Sudan wamechoshana nguvu na Al Ahly ya Misri kwa kufungana mabao 2-2.

Simba wamebakiza mechi moja ugenini dhidi ya Al Ahly ambao wana alam 8.

As Vita na Al-Merreikh rasmi wameshindwa kuendelea hatua ya robo fainali na kuwachia Simba na Al Ahly wakisonga mbele ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya vilabu barani Afrika.