Simba yabadili muda wa kuikabili FC Platnum

0
253

Mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya wenyeji Simba na FC Platinum ya nchini Zimbabwe sasa ni rasmi itachezwa saa 11:00 jioni badala ya 1:00 kama ilivyotangazwa hapo awali.

Muda wa kuanza kwa mchezo huo umerudishwa nyuma baada ya uongozi wa klabu ya Simba kuandika barua kwenda Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kuomba mchezo huo ubadilishwe muda kutokana na jiografia ya mji wa Dar es salaam ulivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa habari wa klabu hiyo, Haji Manara amesema kuwa, baada ya kuandika barua kwenda CAF kuomba mchezo huo kuchezwa saa 11 jioni, Shirikisho hilo limeridhia na kuwapa majibu kuwa sasa mchezo huo utachezwa muda huo badala ya 1:00 jioni.

Amesema kuwa, kilichowasukuma kupeleka maombi hayo ni kutaka mashabiki wengi zaidi kuingia uwanjani kushuhudia mchezo huo, kwani nguvu ya wachezaji wao ipo kwa mashabiki ambao siku zote wamekuwa wakipendelea kikosi chao kupata matokeo mazuri katika uwanja wao wa nyumbani.

“Klabu ya Simba mtaji wake ni mashabiki na ndio mtakaotupa matokeo siku ya mchezo wetu wa marudiano, nguvu ya mashabiki imepelekea klabu zote kubwa za Afrika kushindwa kutamba, hivyo ikiwa tutajitokeza kwa wingi, ndani ya dakika 20 tutakuwa tumeshamaliza mchezo ,”.

“Lakini pia ikiwa tutafuzu basi kizazi hiki cha kina Clatous Chama, Aishi Manula, John Bocco na wengine kitakuwa bora kwani kitakuwa ni kizazi cha kwanza kwenda kufuzu kucheza hatua ya makundi ya Ligi Mabingwa mara ya pili, ni niwahakikishie kwa jinsi morali ilivyo basi ni wazi kazi itakuwa nyepesi kwetu, ” amesema Manara.

Simba inatarajiwa kushika Katika Dimba la Mkapa Jumatano hii kurudiana na FC Platnum Katika mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, ambapo katika mchezo wa awali uliopigwa majuma mawili mjini Harare, FC Platnum waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba.