Simba SC yaifuata Azam FC nusu fainali

0
274

Klabu ya soka ya Simba imetinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam baada ya kuibanjua Dodoma Jiji FC kwa Mabao 3-0 katika mchezo wa nne wa robo fainali ya michuano hiyo kwa mwaka huu.

Simba imeonesha inahitaji nafasi hiyo mwanzoni mwa mchezo huo baada ya nahodha wa timu hiyo John Bocco kuiandikia timu hiyo bao la kwanza katika dakika ya 22 kwa mkwaju wa penati baada ya Benard Morrison kufanyiwa madhambi katika eneo la hatari.

Simba inayotetea ubingwa huo iliandika bao la pili dakika ya 41 kupitia kwa John Bocco ambaye kwa sasa anaoneka kuwa katika kiwango bora.

Mpaka timu hizo zinakwenda mapumziko Simba ilikuwa mbele kwa magoli 2-0.

Simba ilijipatia goli la tatu katika dakika ya 71  kupitia kwa Meddie Kagere aliyengia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya John Bocco.

Kwa matokeo hayo Simba inafuzu kwa hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo na itamenyana na Azam FC katika dimba la Majimaji mjini Songea.

Nusu fainali ya pili itapigwa katika dimba la Ali Hassan Mwinyi, Tabora ambapo Yanga SC itakuwa mgeni wa Biashara United ya Mara.