Simba na Yanga kumiliki viwanja karibuni

0
222

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa amevielekeza vilabu vyote nchini kumiliki viwanja vyao, ambapo timu za Yanga na Simba zimeahidi kutekeleza agizo hilo ndani ya kipindi cha miezi sita.

Mchengerwa ametoa maelekezo hayo mkoani Dar es Salaam alipokutana na watendaji wakuu wa vilabu vinavyoshiriki Ligi Kuu, kwa lengo la kujadili namna bora ya kuendesha ligi kwa ubunifu na ushindani.

Amesema mpango wa vilabu kumiliki viwanja vyao ni takwa la kisheria kulingana na Sera ya Michezo nchini.

Pamoja na mambo mengine kikao hicho kimejadili masuala ya kuzingatia weledi, nidhamu na maadili, ambapo Waziri Mchengerwa ameweka wazi kuwa kwa sasa serikali haitakubaliana na vitendo vyovyote vya rushwa na upendeleo katika michezo kwa kuwa vinachangia kuua na kudidimiza michezo.

Amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuendesha michezo kisasa, ili kuleta maboresho makubwa yatakayosaidia kuifikisha Tanzania kwenye ramani ya kimataifa.

Kwa upande wao watendaji hao wakuu wa vilabu vinavyoshiriki Ligi Kuu wamemshukuru Waziri Mchengerwa kwa kuja na mpango wa kuwashirikisha ili waweze kujadili changamoto zao na serikali, na kupata ufumbuzi wa pamoja na wa kudumu.