Serikali yasema Ndondo Cup itafanyika

0
418

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amesema kuwa mashindano ya mpira wa miguu, Ndondo Cup, yatafanyika kama ilivyopangwa.

Taarifa yake imekuja saa chache baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kusema kuwa mashindano hayo hayajapewa kibali cha kufanyika kama ambavyo imekuwa ikitangazwa.

Akijibu swali la mtumiaji wa mtandao wa Twitter, Fortunatus Buyobe, Naibu Waziri amesema jambo hilo halina ugumu wowote.

“Jambo halina ugumu wowote hili Comrade, taratibu zitafuatwa na mashindano yatafanyika. Uzuri muda bado upo,” ameeleza Mwinjuma.

Kwa upande wake Mratibu wa Ndondo Cup, Shaffih Dauda amesema mashindano hayo ambayo yamefanyika kwa miaka tisa yamekuwa yakisimamiwa na Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), na kwamba kama bado hawajapeleka taarifa TFF, kuna muda wa miezi miwili, hivyo wapo ndani ya muda.