Serikali yaipongeza Simba kutinga robo fainali CAFCC

0
655

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza Klabu ya soka ya Simba kwa kuendelea kuiwakilisha vema Tanzania katika michuano ya Kimataifa kupitia Kombe la Shirikisho barani Afrika (FAFCC).

Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo leo Aprili 6,2022 bungeni jijini Dodoma wakati akisoma hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge kwa mwaka 2022/2023.

“Kipekee niipongeze timu ya Simba SC kwa kupeperusha bendera ya Taifa letu katika mashindano ya Shirikisho la Klabu Afrika, mwenye macho haambiwi tazama, sote tumeshuhudia wakiendelea kuupiga mwingi na kutuwakilisha vema katika medani za kimataifa”. Amesema Waziri Mkuu.

Simba SC ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania ambao wanatarajiwa kumenyana na Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Wekundu hao wa Msimbazi wataanzia nyumbani Aprili 17, kabla ya kusafiri kwenda Houghton jijini Johannesburg kwa mchezo wa marudiano Aprili 24, 2022.

Simba SC wamefanikiwa kwenda Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya US Gendamarie ya Niger katika mtanange uliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita.