Wachezaji 24 wa Serengeti Boys wanaoshiriki mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri chini ya miaka 17 (AFCONU17) wamepimwa vipimo mbalimbali vya magonjwa ya moyo ikiwa ni sehemu ya matakwa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Upimwaji huo umefanyika katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambapo endapo yeyote atakutwa na tatizo wataanza tiba mapema na kama hawa watafuata ushauri wa wataalamu wa afya jinsi ya kutunza mioyo yao.
JKCI ni hospitali pekee nchini iliyothibitishwa na CAF kuwa inakidhi vigezo vyote vya upimaji wa magonjwa ya moyo.
Mbali na Tanzania, nchi nyingine zilizofuzu mashindano hayo ni Mali, Senegal, Ivory Coast, Nigeria, Zambia, Afrika Kusini, Uganda, Algeria, Morocco, Cameroon na Congo.
Tanzania ipo Kundi B pamoja na Congo, Nigeria na Algeria katika mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika nchini Morocco kuanzia Machi 13 hadi Machi 31 mwaka huu.