Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema kuwa halikupokea na wala halihusiki na matumizi ya fedha TZS bilioni 1 iliyotolewa na Rais John Magufuli kufanikisha fainali za AFCON kwa vijana chini ya miaka 17.
“TFF inaendelea kusisitiza kuwa hakuna fedha yoyote iliyopokea wakati wa fainali hizo,” taarifa ya shirikisho hilo imeeleza.
TFF imetoa ufafanuzi huo kufuatia kuwepo taarifa kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema shirikisho hilo limetumia vibaya baadhi ya fedha zikiwemo zilizotolewa na Rais kwa ajili ya fainali hizo zilizofanyika nchini 2019.
Mkurugenzi wa TAKUKURU, Brigedia John Mbungo amesema kwamba baadhi ya watuhumiwa kutoka TFF wamekwishaitwa na kuhojiwa, na nyaraka mbalimbali zimechukuliwa.
Ameongeza kwamba watu hao wana hiari ya kurejesha fedha ama kusubiri uchunguzi ukamilike.
TFF imesema inaamini suala hilo likikamilika itabainika fedha hizo ziliingia katika akaunti ipi pamoja na matumizi yake.