Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Pindi Chana ameagiza kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi watumishi wanaohusika na uendeshaji wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, kutokana na kujirudia kukatika kwa umeme wakati wa michezo.
Kufuatia agizo hilo, Katibu Mkuu, Said Yakubu amewasimamisha kazi Salum Mtumbuka, Kaimu Meneja wa Uwanja, Manyori Kapesa, Mhandisi wa Umeme na Tuswege Nikupala, Afisa Tawala ili kupisha uchunguzi.
Aidha, Yakubu amewasimamisha kazi watendaji wengine wanne ambao nao wana jukumu la uendeshaji wa uwanja ambao ni Gordon Mwangamilo, Gabriel Mwasele, Yanuaria Imboru na Dkt. Christina Luambano.
Kufuatia hatua hizo, katibu mkuu amemteua Milinde Mahona kuwa Kaimu Meneja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, uteuzi unaoanza leo Mei Mosi 2023.
Pia, ameelekeza michezo kwenye uwanja huo ichezwe wakati wa alasiri au jioni badala ya usiku kwa kipindi chote hadi hapo ukarabati mkubwa wa uwanja utakapofanyika.
Umeme katika uwanja huo ulikatika jana wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Yanga na River United ya Nigeria na kupelekea mchezo kusimama kwa zaidi ya dakika 20. Aidha, itakumbukwa tukio hilo lilitokea pia wakati wa mchezo wa Tanzania na Uganda wa kuwania kufuzu AFCON 2023, na kupelekea mchezo kusimama kwa zaidi ya dakika 30.