Wazee wa Mpapaso, Ruvu Shooting FC wameondoka na alama tatu kutoka Uwanja wa Mkwakwani, Tanga baada ya kuwasulubu Wagosi wa Kaya, Coastal Union FC kwa magoli 3-1.
Ruvu Shooting ndio walikuwa wa kwanza kufungua kapu la magoli kupitia kwa Pius Buswita dakika ya 17, na dakika tano baadaye Coastal Union ilisawazisha kupitia kwa Vicent Vicent.
Hata hivyo, Mpapaso uliendelea na Haruna Chanongo aliifungia Ruvu Shooting goli la pili dakika ya 31 na Samson Joseph alihitimisha karamu ya magoli dakika ya 80 ya mchezo.
Licha ya ushindi huo, Ruvu Shooting inabaki nyuma ya Coastal Union ambayo ipo nafasi ya 10 ikiwa na alama 21, wakati vijana wa Mabatini wakiwa nafasi ya 11 na alama 20 kibindoni wakiwa wamepanda kutoka nafasi ya 13.
Mapema saa nane mchana ulipigwa mchezo mmoja uliokutanisha Mbeya City FC na Kagera Sugar FC ambapo Wana Nkurukumbi walifanikiwa kuondoka na ushindi mwembamba wa goli 1-0 dhidi ya wenyeji wao.
Kagera Sugar ipo nafasi ya sita ikiwa na alama 24 huku Mbeya City ikiwa nafasi ya tano ikiwa na alama 25 baada ya timu zote kushuka dimbani mara 18.