Ronaldo na Higuain wamaliza ukame wa magoli

0
2065

Kwenye Seria A nchini Italia, nyota wawili Cristiano Ronaldo na Gonzalo Higuain wamemaliza ukame, baada ya kufunga kwa mara ya kwanza kwenye michezo yao ya ligi tangu kuanza kwa msimu huu.

Kwenye dimba la Allianz mjini Turin, mwanasoka bora duniani Cristiano Ronaldo amemaliza ukame wa mabao baada ya kufunga mabao mawili yaliyoipa Juventus ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Sassuolo.

Ronaldo alizitikisa nyavu katika dakika za 50 na 65 na kumaliza ukame wa kucheza michezo mitatu mfululizo ya ligi ya Seria A bila kufunga bao tangu ajiunge na kibibi kizee cha Turin, akitokea Real Madrid katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.

Huko Sardegna Arena, mshambulaiji mpya wa AC Milan, – Gonzalo Higuain na yeye amefunga goli la kwanza tangu ajiunge na miamba hiyo ya Italia na kufanikiwa kuipa sare ya bao moja kwa moja AC Milan mbele ya Cagliari.

Higuain ambaye hakufunga bao hata moja katika michezo yake miwili ya kwanza tangu atue San Siro kwa mkopo akitokea Juventus, aliisawazishia Milan katika dakika ya 55 baada ya Joao Pedro kuitanguliza Cagliari mapema katika dakika ya nne.

Alama hiyo moja waliyoipata AC Milan inawapandisha hadi katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Seria A wakiwa na alama nne katika michezo mitatu waliyocheza huku wakiwa na mchezo mmoja wa kiporo mkononi.